Washauri kulinda kilimo cha asili

MTANDAO wa Bayoanuai Tanzania umeshauri wakulima kulinda na kuendeleza kilimo cha asili ili kuendelea kuwa na uhuru wa matumizi ya mbegu za asili kwa usalama wa chakula na lishe.

Mtaalam wa Mbegu kutoka katika mtandao huo, David Manongi amesema hayo katika warsha ya mbegu asili iliyofanyika mkoani Dar es Salaam.

Amesema mbegu za asili ni thabiti, himilivu na za uhakika hata katika majanga kama ukame na magonjwa, hivyo ni muhimu zikalindwa.

“Katika mfumo wa mbegu unaosimamiwa na wakulima ,hutumia mbegu ambazo kwa kweli ni thabiti kwa tabia, zinazopandwa kwa zaidi ya msimu mmoja ambazo wamezichagua na wapo huru kuzizalisha, kubadilishana au kuuza” amesema Manongi.

Amesema mbegu za wakulima ni chanzo kikuu cha nasaba za mimea zinazotumiwa na watafiti na kwamba kutokana na hali ya kimaisha ya wakulima wadogo, inawezesha watu binafsi, kaya au vikundi vya wakulima kubadilishana mbegu kwa mbegu.

Naye Mtaalamu mwingine Paul Chilewa ametahadharisha kuwa ukosefu wa chakula bora huweza kusababisha kupata magonjwa yasiyo ya kuambukiza kutokana na ukosefu wa viini lishe katika mazao.

“Kupotea kwa mbegu za asili kunatokana na uhamasishaji wa matumizi ya mbegu zilizoboreshwa na baadhi kutupa mbegu za asili lakini mimi niwaambie siyo kila cha asili ni kibaya,” amesema Chilewa.

Amesema mazao yanayozalishwa kwa mbegu asili ni tiba ya magonjwa mengi hivo kushauri wadau mbalimbali ikiwemo wakulima wenyewe kujikita katika kilimo kwa kutumia mbegu asili.

Amesema upo umuhimu wa kuzilinda mbegu za asilia katika sheria zetu za mbegu akitolea mfano wa baadhi ya nchi ambazo zina sheria bora kuhusu ulinzi wa mbegu zao kama vile Ethiopia, Zimbabwe na Uganda.

Ameelezea shughuli za wadau katika kuhamasisha matumizi ya mbegu asilia Chilewa kuwa ni kuimarisha mitandao na ushirikiano na mashirika mengine juu ya masuala ya haki za mbegu katika ngazi ya kitaifa na kimataifa ikiwa ni pamoja na kuanzisha kikundi kazi cha mbegu za mkulima.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top