WANAFUNZI WAFUNDISHWA JINSI YA KUPAMBANA NA UKATILI WA KIJINSIA

Wanafunzi wa Shule ya Msingi Bombambili iliyopo eneo la Bombambili Kata ya Kivule Wilaya ya Ilala jijini, leo wamefundishwa namna ya kupambana na ukatili wa kijinsia ikiwa ni sehemu ya siku 16 za kupinga ukatili duniani.

Wanafunzi hao wamepata elimu hiyo kutoka kwa wanaharakati wa Kituo cha Taarifa na Maarifa (KC) cha Kata ya Kivule kilichopo chini ya Mtandao wa Jinsia Nchini (TGNP).

Katika mafunzo hayo mgeni rasmi alikuwa Mwalimu Siwema Makene aliyemwakilisha Afisa Elimu wa Kata ya Kivule ambapo alikipongeza kikundi hicho kwa kupeleka elimu hiyo kwenye wanafunzi wa kata yake pamoja na kuibua changamoto mbalimbali kwenye kata hiyo.

Kwa upande wa uongozi wa shule hiyo uliwakilishwa na Mwalimu Sekela Boniface ambaye alikishukuru kikundi hicho kilichopo chini ya TGNP kwa kupeleka mafunzo hayo kwenye shule hiyo ambayo imeshakumbana changamoto za watoto kufanyiwa ukalitili wa kijinsia mara kadhaa.

Mwalimu Sekela amesema watoto baada ya kupata mafunzo hayo sasa wameshaondolewa hofu na kuelekezwa namna ya kuyaripoti matukio hayo na kutajiwa namba 116 ambayo watatakiwa kupiga bila woga endapo watahisi kufanyiwa ukatili wa kijinsia kama vile kupigwa vipigo visivyo vya kawaida, kushawishiwa kufanya ngono na mengineyo. Aliendelea kusema;

“Watoto wengi hapo awali ilikuwa unamkuta tu mtoto amepooza ghafla tofauti na siku za nyuma na ukijaribu kumdodosa wengi walikuwa waoga kusema ukweli kwa kuwaogopa watu wanaowafanyia vitendo hivyo labda mpaka umbane sana ndiyo atakuambia, sasa elimu itasaidia sana kupunguza changamoto hiyo baada ya kuwapa watoto hawa ujasiri wa kuripoti matendo hayo”.

Leave a Comment

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Scroll to Top