Kikongwe wa Miaka 119 Atelekezwa na Wanawe, Polisi Aingilia Kati

Written by on March 3, 2024

Bi. Stamili Endelea Kaloloma ambaye ni kikongwe wa miaka 119, mkazi wa Misegese wilaya ya Malinyi mkoani Morogoro, ametelekezwa na watoto wake wapatao watano ambao hawataki kumtunza wala kumpatia mahitaji yake muhimu licha ya kufikishwa kwenye vyombo vya sheria kupewa maagizo ya kumtunza kutokana na umri wake, badala yake wamemuacha apambane mwenyewe.

Hali hiyo imemfanya Polisi Kata wa Kata hiyo Mkaguzi Msaidizi wa Polisi Michael Rasha, kuingilia kati na kufika kwa Bibi huyo Machi 1, 2024 ili kuona namna ya kumfanya kikongwe huyo aweze kusaidiwa.

Mkaguzi Rasha aliamua kuwaita watoto wa Bibi huyo ambao wanaishi maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye Majiji makubwa pamoja na kuwashirikisha Maafisa Ustawi wa Jamii ili kuhakikisha Bi Stamili anapata matunzo pamoja na haki zake za msingi.

Mkaguzi Rasha alisema ni lazima kila mmoja asimame kwenye nafasi yake kwani wazazi wana haki ya kupatiwa huduma zote muhimu kama ambavyo wao walijitoa kuhakikisha watoto wao wanapata mahitaji na kukua kwa afya hadi kufikia hatua ya kwenda kujitegemea wenyewe, Kitendo cha kushindwa kumtunza mzazi ni ukatili lakini pia ni hatari kwa maisha ya mzazi maana kinaweza kupelekea kifo cha mapema.

Majirani wa Kikongwe huyo wamekuwa wakijitahidi kumpa msaada lakini pia kuwasiliana na watoto wa Bibi huyo bila kupata matumaini jambo ambalo liliwafanya wamtafute Polisi Kata anayesimamia Kata hiyo ili kuwatafuta kisheria.

Tagged as

Reader's opinions

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *Current track

Title

Artist